Dondoo ya Mtoaji: Makala hii ni ya nne katika mfululizo wetu wa sehemu tano unaoitwa “COVID-19: Views from the Field.” Bonyeza hapa kusoma utangulizi ulioandikwa na mtengenezaji wa mfululizo huu, Rebekah Ciribassi.
Kuhusu tafsiri: Tafsiri hii isingewezekana bila msaada wa msingi wa Sophia George, lakini kama kuna makosa ya kiuandikaji ni ya mwandishi. Shukrani ya dhati kwake.
Nimeishi Tanzania tangu mwezi wa tatu mwaka 2018, nikiwa nafanya utafiti wa kiethnografia na familia mbalimbali ambazo zina wagonjwa wenye ugonjwa wa kurithi wa damu unaoitwa siko seli. Nilianza kuvutiwa na utafiti huu wa maisha ya kijamii na ya kisiasa kuanzia mwaka wa 2012, nilipojifunza kwa mara ya kwanza kuhusu kundi la wanaharakati wa kisayansi wa Pan-Afrika, pamoja na Watanzania, wanayoipa kipaumbele huduma na utafiti wa ugonjwa wa siko seli barani kote Afrika. Nilitaka kujua: mabadiliko gani ya msingi ya kianthropolojia yanatokea ili kuhamisha nyakati za maingilio ya afya ya dunia kutoka kasi ya haraka ya magonjwa kama HIV na malaria, kuelekea kwenye uambukizaji wa magonjwa ya kurithi. Karibia miaka miwili ya mahojiano na familia, wanaharakati mbalimbali, na wahudumu wa afya ilinifanya nifikirie zaidi utengenezaji wa fikra zinzozingatia wakati wa kimwili kupitia kwa teknologia ya kigenetiki. Janga la korona likaanza.
Kipindi mgonjwa wa kwanza wa korona anatangazwa nchini Tanzania tarehe 16 mwezi wa tatu, nilikuwa nishaacha kufanya mahojiano ya ana kwa ana na kusafiri kwa ajili ya utafiti. Ingawa kulikuwa hamna mtu aliyekuwa na uhakika wa kiwango cha usambaaji, nilikuwa nahofia kuwaambukiza marafiki zangu na washiriki wa utafiti, ambao wengi wao wana upungufu wa kinga mwili au ni wahudumu wa afya wa muhimu katika hospitali mbalimbali. Lakini hata mbali na hatari ya kibiolojia, kulikuwa na kitu kingine kilichokuwa kinanizuia kufanya kazi yangu: janga la korona lilikuwa limerejesha umuhimu wa huduma ya kasi kwa magojwa yanayoambukizwa haraka, kwahiyo kasi ya taratibu ya utafiti wangu wa kiethnografia pamoja na huduma ya magonjwa sugu zikaanza kuonekana kama haziendani.
Sasa, wiki sita baadaye, virusi vimeanza kusambaa kwa kiasi kikubwa Tanzania, na wagonjwa washatangazwa 480. Ndege zote za kutoka nje ya nchi zimefutwa. Japokuwa hakuna amri yoyote ya kuwalazimisha watu wakae ndani au mipango ya kupunguza mizunguko ya watu Tanzania, hali ya kawaida ya maisha imesitishwa. Mimi kama mtafiti wa kiethnografia, nimejikuta katika hali isiyo ya kawaida, ya kuhitaji kujitenga na kutohama ndani ya “field” yangu, na kukaa bila kuweza kufanya kazi yangu ya utafiti. Muda umeingiliana: kasi ya taratibu ya kiethnographia, muda wa kumalizia masomo katika chuo changu, kasi ya uambukizaji wa kigenetiki, na kasi ya Evolution ya kibindadamu—zote haziendani na kasi ya janga hili. Katika kipindi hiki cha mkanganyiko, inakuwa na maana kuuliza kuhusu siasa za mienendo hii tofauti tofauti, hasa zinavyokuwa katika mahali hapa ninapopaita “the field.”
Urithi wa Ukoloni na Historia ya Uenezaji
Katika insha yake ya hivi karibuni, mhadhiri mtanzania Chambi Chachage anaonesha utofauti kati ya baadhi ya makala yanayohusu Coronavirus katika nchi za Ulaya na nchi za Kiafrika. Ulaya, historia zipo nyingi zinazohusu majanga ya zamani ya mlipuko kama haya. “Black Death” iliyosambaa Italy mwaka 1437, “Spanish Flu” iliyokuwepo Ulaya na Marekani mwaka 1918—kuna kina kirefu cha historia ambayo inatumika na waandishi ili watabiri wakati ujao wa COVID-19 katika nchi za magharibi. Lakini, ingawa janga au “pandemic” ni ya kidunia, uenezaji wa ugonjwa huu barani kote Afrika kwa kawaida hauingii kwenye fikra za kihistoria zinazohusu magonjwa mlipuko ya kidunia. Hii siyo kwa sababu ya ukosefu wa taarifa; wanahistoria wachache washawahi kuandika kuhusu majanga huku nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara [1][2]. Kwahiyo siyo kwamba kuna ukosefu wa ujuzi unaosababisha tusiongee kuhusu majanga ya kale huku Afrika. Badala yake, ni swali la mizunguko ya maarifa, na jinsi inavyoingia kwenye kumbukumbu ya kijamii.
Hili silo jambo la kitaaluma pekee yake. Lina maana kwa jinsi Watanzania, na Waafrika kwa ujumla, wanavyoishi na COVID-19. Kabla Korona kuanza rasmi sehemu yoyote Afrika, hapa Dar es Salaam kulikuwa na imani kwamba isingeweza kutokea hapa. Kwa mitandao ya kijamii na mazungumzo ya kawaida, watu walionekana kuambiana: kuna magonjwa ya Kiafrika na kuna magonjwa ya watu wa Ulaya, magonjwa ya watu weusi na magonjwa ya watu weupe. Malaria ni ya Kiafrika. Ukimwi ni ya Kiafrika. Lakini virusi hivi vipya vilionekana tofauti: ugonjwa wa watu weupe, wa Ulaya. Kwa wiki chache ndani ya mwezi wa tatu, badala ya kuitwa mzungu na watu sokoni, niliitwa “Korona” kwa kejeli. Nadharia zinazotegemea ubaguzi wa rangi zilikuja juu ili kueleza kwa nini COVID-19 isingeweza kuvuka mpaka wa kirangi. Kulikuwa na fikira moja iliyokuwepo mtandaoni (Marekani pamoja na Tanzania) kwamba ngozi nyeusi ingeweza kujikinga dhidi ya maambukizi ya korona. Pia fikira zinazohusu mazingira ya kitropiki na jinsi yanavyojikinga dhidi ya virusi zilianza kuzunguka (kuleta mwangwi wa mantiki ya zamani ya ubeberu). Kulionekana kuwa na ufinyu wa fikra juu ya janga linaloweza kuanzia China na Ulaya halafu kuelekea Afrika, hata kama ilitokea hivyo hivyo mara kadhaa karne zilizopita. Kwahiyo, kwa nini kuna huo ukosefu wa fikra?
Wanahistoria wa Afrika wameandika jinsi udaktari wa kikoloni ulivyotengeneza dhana ya “mwili wa Kiafrika” kwa ajili ya ubeberu. Afrika ilijengwa katika ubunifu wa watu wa Ulaya kama uwakilishi wa maradhi, mateso, machafuko, na maambukizo: bara jeusi—“the dark continent”—inayohitaji usafishaji wa daktari mweupe [3][4]. Athari ya kudumu imekuwa ubaguzi dhabiti wa miili ya Kiafrika wakitengwa na kuwekwa kwenye kipengele tofauti cha kibiolojia mbali na watu wengine duniani. Sasa, kipindi cha COVID-19, ubaguzi huo huo umesababisha wahamiaji Waafrika kufukuzwa kwenye nyumba zao nchini China. Udaktari wa kikoloni ulivyobuni dhana ya “mwili wa Kiafrika” kama ishara ya maambukizi yanayotishia watu wa Ulaya walioaminika kuwa wenye afya zaidi, watu walikuja kujua mtiririko wa maambukizi yanaweza kuelekea kwenye mwelekeo mmoja tu: kutoka Afrika kwenda nje, na sio kinyume chake. Pia wakoloni walivyofikiria Afrika kama bara “bila historia,” kama mahali pa kwanza pa kuzaliwa binadamu na mahali nje ya dunia ya “kisasa.” Hivyo, udaktari wa kikoloni umetoa picha ya mwili wa Kiafrika kama mwili bila historia. Hii siyo kusema kwamba udaktari wa kikoloni ulikuwa hauna utofauti wowote barani kote, kwamba ulikuwa bila kipingamizi, au kwamba umeandaa hali ya maendeleo ya udaktari wa Kiafrika tangu hapo. Lakini kuna faida ya kuchunguza urithishaji wa kikoloni ambao umeathiri ukuaji na mwenendo wa janga la COVID-19 Afrika—urithishaji ambao umebeba siasa ya kiwakati.
Hali ya Dharura, Matarajio, na Kujenga Taifa
Kiongozi mkuu wa Tanzania, Rais Magufuli, amelaumiwa kwa jinsi alivyoshughulikia COVID-19 hadi sasa. Mwanzoni, kulikuwa na majibu ya taratibu wakati idadi ya wagonjwa ilikuwa inaanza kuongezeka kidogo kidogo. Kwanza, alisisitiza Watanzania wanawe mikono na waepuke mikusanyiko ya watu wengi, akaanza kulazimisha wasafiri wanaotoka nje ya nchi wajiweke karantini, na akafunga shule zote. Hata hivyo, mpaka leo mipaka ya nchi bado iko wazi, sehemu za ibada, masoko, na usafiri wa umma unaendelea kufanya kazi, na hakuna amri rasmi yeyote ya kukaa ndani wala kuingia ndani mapema, kama amri zilizowekwa katika nchi za jirani. Mara kadhaa, Rais amesisitiza Watanzania waendelea kutoka ili “wachape kazi” kwa ajili ya uchumi wa taifa. Ametoa tahadhari dhidi ya kukubaliana na mikakati ya nchi za nje, na ameonesha tuhuma juu ya vifaa vilivyoletwa nchi za nje kama msaada. Wiki hii tu serikali imeshtaki wafanyakazi wa maabara kuu ya taifa kwamba wamenunuliwa na mabeberu kwa kutoa majibu ya vipimo vya COVID-19 ambayo rais anayodai siyo sahihi. Badala ya kuamini msaada wa kigeni, amependekeza Watanzania wategemee dawa za mitishamba na kujifukiza. Kwahiyo inaonekana kwamba Magufuli anaelewa mgogoro huu kama tishio la uhuru wa utawala wa nchi, na nafasi ya kudai kujitawala kwa Tanzania. Kwa juhudi zake za kuokoa uchumi na kuongeza utaifa, Magufuli amejitahidi kuzingatia historia ya kijadi na wakati ujao, kwa mustakabali wa taifa. Kwa sasa, idadi ya wagonjwa inaongezeka kwa kiwango kikubwa kinachozidi nchi za jirani, na wakosoaji wanamlaumu raisi kwa kutenda kazi yake bila kasi ya dharura inayotakiwa kutumika ili kupunguza maambukizi.
Tathmini nyingi za majibu ya Kiafrika katika janga hili la korona zimeyawakilisha kama majadiliano kati ya wanaotaka “lockdown” (yaani wote kukaa ndani kwa muda mrefu) au wanaokataa lockdown. Kwa mtazamo huu, ni chaguo kati ya hatari za kiuchumi au hatari za kiafya. Lakini ninahisi tunaweza kuelewa zaidi tukiiangalia kama mgongano wa muda. Wito wa kasi ya dharura, ikiwa lockdowns, mida maalum ya kurudi nyumbani (“curfew”), au njia nyingine, cha msingi ni kuzingatia kasi ya haraka ya anguko la afya. Ni wito kutenda kazi kwa haraka, bila uwezo wa kutabiri wiki au miezi inayokuja. Udhoofishaji wa huduma za kijamii Afrika, kuanzia kipindi cha ukoloni na kuongezeka kutokana na Mipango ya Marekebisho ya Kimuundo (“Structural Adjustment Programs”) katika miaka themanini, umesabibisha anguko la mfumo wa afya na kutengeneza huduma za afya ambazo haziwezi kudumu kwa muda mrefu.
Changamoto za kuhudumia wagonjwa wenye COVID-19 nchini Tanzania zinaonesha historia ndefu zaidi ya mfumo unaofanya kazi chini ya “triage” [5]. Katika hali hii, utoaji wa huduma ya afya umetegemea msaada wa miradi ya kimataifa na utafiti wa kuchunguza dawa mpya. Bila kuzingatia hali hii, daktari mmoja mfaransa alihojiwa mwezi wa nne mwaka 2020 na kusema kwamba chanjo cha Korona ipimwe kwa Waafrika. Maoni yake yalisababisha hasira kubwa kati ya Waafrika wengi wa nchi mbalimbali. Mabishano haya yameonesha kiwango ambacho udhoofishaji wa huduma ya afya, kasi ya haraka ya dharura, na uhitaji wa kutoa huduma kwenye mfumo wa afya unaozidiwa unakaribisha ukoloni mamboleo, ubaguzi wa rangi, na hatari. Janga linadai vitendo vya haraka na matokeo ya muda mfupi, lakini huku Afrika, kihistoria, vitendo vya haraka vimekuja na matokeo mabaya ya kujitawala.
Kujitawala na utaifa ni itikadi ambazo zinategemea simulizi fulani za historia na wakati ujao, wakati janga linazingatia wakati uliopo pekee yake: historia na wakati ujao ni anasa ambazo hali hii ya sasa ya kutokuwa na uhakika hairuhusu.
Kuhusu Mgusano wa Kisiasa
“Hakuna ufahamu wa Mwingine ambao usiokuwa pia kitendo cha kiwakati, kihistoria, na kisiasa” (Fabian 1983:1). [6]
Labda kitu cha kuchanganya zaidi kuhusu COVID-19 ni kuingilia na kulazimisha maisha yawe kwenye wakati uliopo pekee yake. Kumbukumbu za kijamii na kufikiria yajayo inakuwa vitendo vya kisiasa mbele ya janga la maambukizi. Kasi ya haraka ya janga inapunguza wigo wa uzingatiaji kwa kuangalia mgusano tu—kitu ambacho inaleta athari za kisiasa.
Wakati huo huo, mgusano wa utafiti wa kiethnografia pia umekuwa hatarishi. Lakini ndani ya hii miezi michache ya karibu, wanasayansi wa kijamii, wanaanthropolojia, na wananadharia wa utamaduni wametakiwa kufanya hitimisho la wakati uliopo kuhusu mienendo ya kijamii na kisiasa ya janga la COVID-19. Kitendo cha ethnografia kwa kawaida kinakuwa taratibu, yaani kuuliza swali moja na kutumia miaka mingi sana kuijibu kabla ya kuandika na kuchapisha hitimisho.
Maisha ya janga hili yamefupisha wakati wa kiethnografia, na sisi tumesajiliwa kwenye juhudi za kimataifa za kupambana na virusi. Ghafla na kwa wakati moja, wanaethnografia tunatakiwa kutulia sehemu moja, na kukubalina njia mpya na za haraka za kufanya na kuwasilisha utafiti wetu. Hayo mabadiliko ni ya maana sio kwa sababu ya ubora wa hitimisho letu tu, lakini pia kwa sababu utafiti wa kiethnografia ni kitendo cha kisiasa cha kufanya na kuzalisha fikra za wakati [7].
Mbele ya hizi changamoto mpya za ethnografia, imekuwa muhimu kukataa taswira ya janga hili linalokuwa bila historia au bila siasa. Wanaethnografia wawe makini kuepuka hali ya uharaka, na kuelewa muda wa mgusano kama uhakikishaji wa muingiliano wa watendaji, kila mmoja mwenye historia zake na nyakati zake. Kwa hiyo, kama ni mgusano wa kiethnografia (ana kwa ana au kupitia teknolojia), mgusano wa kuambukiza, au mgusano wa kuacha urithi wa kigenetiki (kama siko seli), muingliano huu unatoa mifano au kielezo, pamoja na kuzalisha, historia na yajayo ambayo yasiyo ya moja kwa moja na zenye maana za kisiasa.
References
[1] Chouin, Gérard (2018). “Reflections on Plague in African History (14th–19th c.).” Afriques, no. 09. https://doi.org/10.4000/afriques.2228
[2] Killingray, David (2003). A New “Imperial Disease”: The Influenza Pandemic of 1918-9 and its Impact on the British Empire. Caribbean Quarterly 49(4):30-49.
[3] Vaughn, Megan (1991). Curing Their Ills: Colonial Power and Africa Illness. Stanford: Stanford University Press.
[4] Comaroff, Jean (1993). The Diseased Heart of Africa: Medicine, Colonialism, and the Black Body. In Knowledge, Power, and Practice: The Anthropology of Medicine and Everyday Life. Eds. Shirley Lindenbaum (Editor), Margaret M. Lock. University of California Press. Pp. 305-329.
[5] Nguyen, Vinh-Kim (2010). The Republic of Therapy: Triage and Sovereignty in West Africa’s Time of AIDS. Durham: Duke University Press.
[6] Fabian, Johannes (1983). Time and the Other: How Anthropology Makes Its Object. New York: Columbia University Press.
[7] Paul Wenzel, Geissler (2017). “Ethnography as Re-enactment : Performing Temporality in an East African Place of Science.” In How Do Biomedicines Shape People’s Lives, Socialities and Landscapes?, 143rd ed., 187–210. Senri Ethnological Reports. https://doi.org/10.15021/00008649